Shirika la Afya Duniani – WHO limethibitisha kuwa mtoto wa miaka mitano nchini Uganda anaugua ugonjwa wa Ebola.
Hii ni mara ya kwanza kwa mgonjwa wa Ebola kugundulika nchini Uganda, tangu kuzuka kwa ugonjwa huo katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo – DRC, ambayo ni jirani na nchi hiyo.
Mtoto huyo ambaye ni wa kiume inadaiwa alisafiri kwenda DRC akiwa na familia yake Jumapili iliyopita, na alikimbizwa hospitalini baada ya kurejea nchini Uganda na kuonekana kuwa ana dalili za Ebola ikiwa ni pamoja na kutapika damu.
Watu wengine Wanane ambao walikua karibu na mtoto huyo, wakiwemo wale aliosafiri nao, kwa sasa wapo chini ya uangalizi mkali.
WHO imeipongeza Uganda kwa uharaka wake wa kushughulikia taarifa hiyo ya kuwepo kwa mgonjwa wa Ebola nchini humo, hatua ambayo inaweza kusaidia ugonjwa huo kutoenea zaidi.
Zaidi ya Watu Elfu Mbili wamegundulika kuugua ugonjwa wa Ebola katika kipindi cha miezi Kumi iliyopita kwenye Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.