Mtoto wa Idriss Deby kuiongoza Chad

0
456

 
Mahmud Idriss Deby Itno ambaye ni mtoto wa Idriss Deby, Rais Mteule wa Chad aliyefariki dunia hii leo, ametangazwa kuwa kiongozi wa baraza la kijeshi la nchi hiyo litakaloongoza kwa kipindi cha miezi 18.

Mahmud ambaye ni miongoni mwa viongozi wa juu wa jeshi la Chad,  atakuwa na kazi ya kuliongoza Taifa hilo hadi hapo utakapofanyika mchakato wa kumpata Rais mpya.

Habari zaidi kutoka nchini Chad zinaeleza kuwa, tayari Baraza la Mawaziri la nchi hiyo limevunjwa baada tu ya kutangazwa kifo cha Idriss Deby aliyeliongoza Taifa hilo kwa takribani miaka 30.

Kifo cha Idriss Deby kilitangazwa saa chache baada ya Tume ya Taifa ya nchi hiyo kumtangaza mshindi wa kiti cha Urais kwa kipindi cha sita kufuatia uchaguzi uliofanyika tarehe 11 mwezi huu.

Akitangaza kifo cha Idriss Deby, Msemaji wa jeshi la Chad amesema kuwa kiongozi huyo amefariki dunia kufuatia majeraha aliyoyapata wakati wa mapambano baina ya vikosi vya Serikali na waasi katika mpaka wa nchi hiyo na Libya mwishoni mwa wiki.

 Idriss Deby alikuwa katika ziara ya kuvitembelea vikosi vya Serikali ambavyo vimekuwa vikipambana na Waasi hao.