Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema sio haki kwa mataifa duniani kuwabagua, kuwanyanyasa na kuwanyanyapaa raia wa Afrika Kusini ambako kirusi cha Corona kilichobadili tabia kinachojulikana kama Omicron kimegunduliwa.
Kiongozi huyo wa WHO ametoa wito huo huku Wanasayansi wa Afrika Kusini wakisema kirusi cha Omicron pia kilikuwepo katika baadhi ya mataifa ya Ulaya, hivyo hakuna mantiki yoyote ya kuihukumu nchi hiyo.
Marekani, Ujerumani na Mataifa ya Asia zinaendelea kutangaza mikakati mbalimbali ya kupambana na maambukizi mapya ya kirusi hicho.
Marekani imetangaza kutoa dozi milioni 200 za chanjo ya corona kwa mataifa mbalimbali duniani katika kipindi cha siku mia moja zijazo.