Mazishi rasmi ya Rais wa Pili wa Kenya, Mzee Daniel arap Moi, yanafanyika leo nyumbani kwake Kabarak.
Habari kutoka nchini Kenya zinaeleza kuwa, mazishi hayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na takribani watu elfu 30, wengi zaidi wakiwa ndugu, jamaa na marafiki wa familia ya Mzee Moi.
Hapo jana yalifanyika mazishi ya Kitaifa katika uwanja wa michezo wa Nyayo uliopo jijini Nairobi na kuhudhuriwa na wakuu na viongozi waandamizi kutoka nchi mbalimbali.
Miongoni mwa wakuu wa nchi waliohudhuria ni pamoja Rais wa Rwanda, Paul Kagame, Yoweri Museveni wa Uganda, Salva Kiir wa Sudan Kusini, na Ismaïl Omar Guelleh wa Djibout.
Katika mazishi hayo ya kitaifa ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Mzee Benjamin Mkapa na miongoni mwa wajumbe alioambatana nao alikuwamo Rais mstaafu wa awamu ya nne, Dkt Jakaya Kikwete.