Mgomo wasitisha shughuli Ubelgiji

0
925

Karibu safari zote za ndege mjini Brussels nchini Ubelgiji zimefutwa kutokana na mgomo wa wafanyakazi wanaodai nyongeza ya mishahara.

Wafanyakazi wa Shirika la Ndege la Ubelgiji na wale wa viwanja vya ndege nchini humo wamegoma kufanya kazi na mgomo wao utaendelea hadi siku ya Ijumaa wiki hii, ikiwa ni hatua ya kushinikiza waajiri wa wafanyakazi hao kuchukua hatua za haraka.

Awali katika taarifa yake, Shirika la Ndege la Ubelgiji lilisema kuwa halitoruhusu ndege kuingia ama kutoka nchini humo kwa kuwa halijui ni wafanyakazi wangapi wangefika kazini kutoa huduma.

Habari kutoka nchini Ubelgiji zinasema kuwa, hali ni mbaya zaidi katika mji mkuu wa nchi hiyo Brussels ambako mkutano wa Mawaziri wa Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO) ulitarajiwa kufanyika.

ayo kampuni ya Reli ya nchi hiyo imefuta nusu ya safari zake katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo, huku usafiri wa treni za mwendo kasi kutoka London nchini Uingereza na Paris nchini Ufaransa ukiendelea kama kawaida.

Habari zaidi kutoka nchini Ubelgiji zinasema kuwa wafanyakazi wa sekta ya afya pia wamejiunga katika mgomo huo, huku askari polisi nao wakielekea kuwaunga mkono wafanyakazi wengine katika mgomo huo.