Mgomo wa Wafanyakazi wa usafiri wa anga nchini Kenya umeendelea na kusababisha baadhi ya ndege kuelekezwa kutua katika nchi jirani.
Wafanyakazi hao wamegoma kupinga mpango wa serikali ya Kenya wa kuweka shughuli za usimamizi wa uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta chini ya Shirika la Ndege la nchi hiyo na Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja wa Ndege (KAA).
Wafanyakazi hao wanapinga mpango huo kwa madai kuwa huenda ukachangia wengi wao kukosa ajira.
Mgomo huo umesababisha maelfu ya abiria kukwama katika viwanja vikubwa vya ndege kikiwemo hicho cha Jomo Kenyatta baada ya ndege sitini kushindwa kuhudumiwa.
Viwanja vingine vya ndege vilivyoathiriwa na mgomo huo wa wafanyakazi wa anga nchini Kenya ni Mombasa, Eldoret na Kisumu.
Serikali ya Kenya imeulaani mgomo huo wa Wafanyakazi wa Usafiri wa anga na kusema kuwa ni batili na kukiomba kikosi cha jeshi la anga cha nchi hiyo kusaidia kukabiliana na hali hiyo.
Awali askari wa kutuliza ghasia nchini Kenya walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafanyakazi hao waliogoma, ambao walikua katika vikundi.