Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limethibitisha kufutwa kwa mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwaka 2019 nchini Cameroon, kati ya Kenya na Sierra Leone.
CAF imesema kuwa mchezo huo wa kundi F uliokuwa uchezwe Jumapili ya wiki hii jijini Nairobi, umefutiliwa mbali kutokana na Sierra Leone kuendelea kutumikia adhabu ya kufungiwa kwa muda usiojulikana na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).
Tayari CAF imeviandikia barua vyama vya soka vya nchi zote mbili kuviarifu juu ya mchezo huo kufutwa ikiwa ni maagizo kutoka FIFA ambayo ndiyo mamlaka ya juu zaidi ya soka duniani.
Mwezi oktoba mwaka huu, bodi ya CAF ilifuta michezo miwili kati ya Sierra Leone na Ghana iliyokuwa ichezwe nyumbani na ugenini na kuondoa kabisa uwezekano wa mechi hizo kuchezwa hata kama adhabu ya Sierra Leone itaondolewa.
Hata hivyo CAF bado haijaweka wazi nini kitaendelea baada ya kufutwa kwa mchezo huo na kwa kiasi gani utaathiri kampeni za mataifa husika katika kundi hilo kwenye kufuzu kwa michuano ya AFCON.
Mpaka sasa Kenya wanaongoza kundi F wakiwa na alama saba wakati Ghana, Ethiopia na Sierra Leone kila mmoja wakiwa na alama moja.