Mbunge Kenya ashtakiwa kwa tuhuma za mauaji

0
393

Mapema leo, mbunge wa Embakasi Mashariki, akiwa amekanusha tuhuma zinazomkabili za jaribio la mauaji ya mcheza muziki (DJ) jijini Nairobi, na kubeba silaha (bunduki) akiwa amelewa.

Babu Owino amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kilimani leo katika kesi iliyokuwa ikiongozwa na Hakimu Mkazi Francis Andayi kufuatia tukio lililotokea Ijumaa Januari 17 mwaka huu ndani ya B-Club.

Owino ambaye jina lake rasmi ni Paul Ongili anatuhumiwa kujaribu kumuua kwa kumpiga risasi shingoni Felix Odhiambo Orinda kinyume na kifungu namba 222 cha Kanuni za Adhabu.

Mbunge huyo amepelekwa rumande hadi Januari 27, kesi yake itakaposikilizwa tena kwa ajili ya kusikiliza majibu ya maombi ya dhamana, baada ya kunyimwa dhamana leo kwa kile upande wa jamhuri ulichodai kuwa ataathiri uchunguzi wa kesi hiyo.

DJ Orinda anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Nairobi alipokimbizwa dakika chache baada ya tukio hilo kutokea.

Owino alikamatwa siku hiyo hiyo akiwa hospitalini akisubiri Orinda kutibiwa, na Jumamosi alihamishwa kutoka Kituo cha Kilimani na kwenda Kituo cha Polisi Gigiri kwa lengo la kuepuka vurugu kwenye kituo.