Mbegu za uzazi zafikisha watoto 550

0
293

Mwanaume mmoja raia wa Uholanzi anadhaniwa kuzaa watoto zaidi ya 550 kulingana na mbegu za uzazi alizotoa na hivyo kuamriwa kuacha kutoa mbegu hizo.

Kuna uwezekano kwa mwanaume huyo Jonathan M (41) kutozwa faini ya Pauni elfu 88 ambazo ni zaidi ya shilingi Milioni 256 za Kitanzania endapo ataendelea kuchangia mbegu zake za uzazi.

Mahakama mjini The Hague ilimtaka Jonathan
atoe orodha ya kliniki zote alizokuwa ametuma mbegu zake na kuamuru kuharibu kwa mbegu hizo.

Miongozo ya Kimatibabu nchini Uholanzi inamtaka mtu anayetoa mbegu za kiume za uzazi kutokuwa na watoto zaidi ya 25 katika familia 12, lakini Jonathan amesaidia kuzaliwa kwa watoto kati ya 550 na 600 tangu alipoanza kutoa mbegu hizo mwaka 2007.

Mwaka 2017 Jonathan M alipigwa marufuku kuchangia mbegu zake za uzazi katika kliniki mbalimbali nchini Uholanzi baada ya kubainika kuwa alikuwa amekwishasaidia kuzaliwa kwa watoto zaidi ya 100.

Hata hivyo inaelezwa kuwa mwanaume huyo aliendelea kuchangia mbegu zake za uzazi katika kliniki za nje ya nchi ya Uholanzi na kupitia mitandaoni.