Sri Lanka imefanya mazishi ya kwanza ya pamoja ya watu waliokufa katika mfululizo wa mashambulio ya mabomu ya kujitoa muhanga, yaliyotokea kwenye Makanisa na hoteli kadhaa wakati wa Sikukuu ya Pasaka.
Mazishi hayo ya pamoja ya miili ya watu Thelathini, yamefanyika katika kanisa la Mtakatifu Sebastian, lililopo kwenye mji wa Negombo, kanisa ambapo nako kulitokea shambulio la bomu la kujitoa muhanga.
Mazishi hayo yamefanyika wakati Sri Lanka ikifanya maombolezo ya siku moja, kuwakumbuka watu wote waliokufa katika tukio hilo.
Wakati hayo yakiendelea, Polisi nchini Sri Lanka wamesema kuwa idadi ya watu waliokufa katika mashambulio hayo imeongezeka na kufikia 310 na wengine takribani Mia Tano wamejeruhiwa.
Serikali ya Sri Lanka inakishutumu kikundi cha Kiislam cha Thowheed Jamath (NTJ) cha nchini humo kwa kuhusika na mashambulio hayo kwa kusaidiwa na vikundi vingine vikubwa vya kigaidi.
Hadi sasa watu 40 wanashikiliwa na Polisi nchini Sri Lanka kwa tuhuma za kuhusika na mashambulio hayo ya mabomu ya kujitoa muhanga kwenye Makanisa na hoteli kadhaa nchini humo.