Malaysia yakataa kuwa dampo la dunia

0
333
Nchi ya Malaysia yapambana vikali kutunza mazingira kwa kurudisha taka za plastiki kwenye nchi zilipotoka taka hizo. Picha: Phys.org

Waziri wa Mazingira wa Malaysia, Yeo Bee Yin akiwa kwenye ziara Pengani, leo, Januari 20 amesema kuwa makontena 110 ya taka yaliyoingizwa nchini humo kutoka nchi mbalimbali yatarudishwa kwenye nchi husika.

Malaysia ilifanikiwa kurudisha makontena 150 ya taka za plastiki kwenye nchi 13 katika robo ya mwisho ya mwaka 2019, na zoezi hilo bado linaendelea.

“Msimamo wetu ni thabiti. Tunataka kuzirudisha (taka) na pia tunatuma meseji kwamba Malaysia sio shimo la taka la ulimwengu.”

Yeo amesema wenye mpango wa kuifanya nchi hiyo dampo la taka “waendelee kuota,” wakati akiongea na waandishi wa habari katika bandari ya kaskazini mwa Pengani.

Makontena hayo 110 yanatarajiwa kusafirishwa katikati ya mwaka huu, huku Marekani ikitarajiwa kurudishiwa kontena 60 mbali na mengine 17 yaloyorudishwa mwaka jana.

Mbali na Marekani, Canada ambayo awali ilirudishiwa makontena 10 itarudishiwa makontena mengine 15. Wakati huo huo, Japan, Uingereza na Ubelgiji zinatarajiwa kurudishiwa makontena 14, 9 na 8 mtawalia.

Hatua hii imetumika katika mpango wa nchi hiyo kuachana na matumizi ya plastiki ili kulinda mazingira.