Malawi yathibitisha Makamu wa Rais kufariki dunia

0
470

Vikosi vilivyokuwa vikiitafuta ndege iliyombeba Makamu wa Rais wa Malawi, Saulos Chilima na watu wengine tisa wamefanikiwa kupata ndege hiyo na hakuna aliyepatikana akiwa hai.

Akilihutubia Taifa muda mfupi uliopita, Rais Lazarus Chakwera wa Malawi amesema ndege hiyo ilianguka katika eneo la Msitu wa Chikangawa huko Mzimba.

Ndege hiyo ambayo ni mali ya Jeshi la Ulinzi la Malawi ilitoweka kwenye rada baada ya kuondoka katika mji mkuu wa nchi hiyo Lilongwe jana asubuhi.

Ilitakiwa kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mzuzu, Kaskazini mwa nchi hiyo baada ya saa nne asubuhi kwa saa za Malawi, lakini haikuonekana.

Makamu huyo wa Rais wa Malawi alikuwa akielekea kuiwakilisha Serikali katika mazishi ya Waziri wa zamani wa Malawi, Ralph Kasambara, aliyefariki dunia siku chache zilizopita.