Simulizi namna taka za Plastiki zimekuwa mkombozi kwa Jamii

0
615

Ni rahisi kuidharua kazi ya chupa za plastiki (makopo), lakini wengi wao wanadai inawalipa na inawabadilishia maisha.Udadisi wa mwandishi wa Habari hii kwa baadhi ya akina mama na vijana waliounda kikundi cha pamoja huko Tabata mkoani Dar ar es Salaam ambao kazi yao kubwa ni kuokota chupa za plastiki kwaajili ya kuzirejeleza walisema Kuna ahuweni wanapata kupitia kazi hiyo.

Ni kikundi, kilichosajiliwa na serikali tangu mwaka 2021, kina wanawake 11 na wanaume 3  lengo lao kubwa  ni kuokota na kukusanya chupa za plastiki  kwa lengo la kuweka mazingira safi.

Kutokana na uzuri wa jambo hilo, mwandishi wa habari hizi alifika mpaka eneo wanakofanyia kazi kufahamu kwa kina kwanini waliamua kuunda kikundi hicho, na yapi hasa malengo yao kwa miaka ijayo, ni zipi changamoto wanazokumbana nazo.

Mwandishi wa habari hii alipofika kwenye kiwanda chao,  aliona   shehena kubwa ya lundo la chupa zilizopangwa kwa mtiririko na kwa makundi.

Wanakikundi hao baada ya kutambua ugeni uliofika ofsini kwao ni mwandishi wa habari ghafla nyuso zao ziligeuka kuwa na tabasamu mmoja kati yao akasikika akisema ‘bora mwandishi wa habari umekuja kilio chetu kiifikie serikali.

Shughuli kuu inayofanyika mahali hapo ni kukusanya chupa za plastiki zilizotupwa na watu baada kupata kinywaji au shughuli mbalimbali  kisha wanazifikisha hapo kwaajili ya kuzichakata.   

Mmoja wa Wanakikundi hicho, Rehema sanga, anasema awali kabla ya kuwa na ofisi hiyo walikuwa wanakusanya  na kwenda kuzitupa kwenye dampo bubu na mitaroni baadaye walipata ufadhili ili kuboresha ufanyaji kazi wao.

“Tuliona uchafu ulikuwa umezagaa, watu wengi walikuwa wanatupa makopo hayo mengine ndani yanamikojo yanatoa uchafu na harufu mbaya baada ya hapo tukapata ufadhili kutoka kwenye taasisi ambayo kwa sasa imetuacha.

“Wakati mwingine tulikuwa tunakwenda kuyauza unaokota makopo mengi lakini unauza kg moja sh 300 ilikuwa hailipi lakini tangu tuunge hicho kikundi anagalau kwa Sasa tunapata chochote kitu” anasema

Rehema anaendeleza ufafanuzi wake kwamba  walifanikiwa kubadili maisha kwa kiasi, lakini tangu mfadhili wao wa awali alipojitoa imekuwa chagamoto kubwa sana kupata kipato cha kukidhi mahitaji ya nyumbani.

Muokota makopo mwingine katika kikundi hicho, Halima mudi, anasema awali wakati wanaanzisha kikundi hicho walikuwa na maisha magumu baadaye wakatafuta mfadhili wa kuwajengea kibanda ili wapate sehemu ya kuhifadhia taka. Ameongeza kuwa kazi hiyo imebadilisha maisha kwa kiasi kwa kuwa awali alikuwa anashindwa kusomesha watoto wake, lakini baada ya kupata ufadhili waliweza kumudu.

Kwa upande wake Salama anasema malengo yao ni kuyafikia maeneo mengine ili kuhakikisha jiji linakuwa safi kama serikali inavyosistiza hivyo kwa sasa wanaangalia namna ya kuanzisha bishara itakayo waingizia pesa kama ikitokea wamekosa wafadhili ili waweze kusimama wenyewe kwa kuwa wanaipenda kazi hiyo kutoka moyoni.

Pamoja na kufanya kazi hiyo kwa kipindi kirefu Rehema anasema,  viongozi wa eneo hilo waliofika na kutembelea kikundi chao ni Mbunge wa Jimbo hilo na diwani wa kata waliyopo.

Hata hivyo,  anakiri wapo hatarini kupatwa na maradhi kutokana na kukosa vifaa muhimu kama gloves, na buti pale wanapookota taka na hivyo wanaiomba serikali na wadau wa mazingira  kuwaangalia kwa jicho la tatu kwa kile wanachofanya kwenye mazingira.

Salama kinyamagoha, anasema tangu waanze kazi hiyo kwenye eneo wanalofanyia kazi wamefanikiwa kupunguza makopo  kwa aslimia 90 akitofautisha na awali na kwamba maeneo yote wanakopita hakuna uchafu wa chupa unaozagaa.

MAHITAJI YA WANAKIKUNDI HAO

Waokota taka hao, ambao ndani yao kuna mchanganyiko wa kina mama na vijana wamewaomba wadau na serikali  kuwasaidia eneo jingine kwaajili ya kukusanyia taka kwa kuwa eneo walilopo kwa sasa ni mali ya mtu binafsi na kwamba siku litakapohitajika watakosa mahali pakufanyia kazi na wanaweza kusitisha huduma hiyo ambayo ni muhimu kwa ustawi wa mazingira.

Vilevile, wanahitaji mkopo toka serikalini na tasisi za fedha zinazokopesha ili waweze kujiinua kiuchumi mmoja mmoja na kwamba wanasifa zote kwakuwa kikundi chao kimesajiliwa serikalini.

MAONI YA VIONGOZI WA SERIKALI

Mkuu wa Wilaya Ilala, Edward Mpogolo amekiri kuvifahamu vikundi vya waokota taka katika eneo lake la kazi na kusema kuwa Serikali imekuwa ikivisaidia vikundi vya namna hiyo kwa njia nyingi ikiwamo kuwapa mikopo. Amesema shughuli inayofanywa na waokota makopo imeleta matokeo chanya katika usafi wa mazingira nakussisitiza kuwa wanapaswa kuungwa mkono na serikali.

Mpogolo ameongeza kuwa ikiwa watanzania na wana Ilala wakikubali kwamba taka ni mtaji na sio uchafu hakuna mahali patakuwa pachafu kwa kuwa watazigeuza fursa kama ilivyo kwa waokota makopo walivyoigeuza fursa kazi yao.

“Leo hii, hakuna mtu anapiga kelele kuhusu chupa hata ukitupa barabarani ndani ya dakikaka 15 unakuta haipo imeshaokotwa, Kikubwa ni kuangalia namna gani wanapofanya kazi hiyo wanakuwa salama kiafya.

Tunacho wasaidia ni kuwapa elimu, kwa kushirikiana na taasisi nyingine, wale waliosajiliwa tunawapa mikopo ile ya asilimia kumi kama ni wanawake wanakwenda kwenye kundi lao, vilevile walemavu na vijana, pamoja na kuwasaidia maeneo ya kuhifadhi chupa zao baada ya kuziokota kabla ya kwenda kuyeyushwa kiwandani.’’ Amesema Mpogolo

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Uthibiti Taka na Usafishaji Wilaya ya Ilala, Rajabu Ngoda amesema  huwa wanatoa elimu kwa kina mama ya kutambua kama taka ni mali na inawezekana kuzigeuza fursa na kuapata fedha. Amebainisha pia kuwa huwa wanawapa elimu ya kuzitenganisha chupa za plastiki na taka za aina nyingine ili kufanikisha mchakato wa urejezaji.

Alipoulizwa kuhusu kuhusu mpango wa seriakli kukisaidia kikundi hicho, alikiomba kifike ofsisini kwao wakapatiwe mikopo kwa kuwa ipo mikopo ya serikali ambayo wanaweza kuipata ili kununua vifaa vinavyoweza kuwasaidia kwenye shughuli zao.

“kwa sababu wanakikundi na wamekisajili, kuna mikopo ya vijana, akina mama, walemavu ya asilimia kumi, kwa hiyo waandike andiko lao vizuri watu wa maendeleo ya ustawi wa jamii watawasaidia watapata mikopo na kukuza wanachokifanya” amesema Ngoda