Afisa Maudhui wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dominic Mgaya amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa kosa la kuchapisha maudhui mtandaoni bila kuwa na leseni ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Akisoma hati ya mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo RIchard Kabate, wakili wa Serikali, Adolf Ulaya amesema kuwa mshitakiwa anakabiliwa na kesi ya jinai namba 127 ya mwaka 2020.
Mgaya anadaiwa kurusha maudhui kupitia ukurasa wa YouTube wa CHADEMA MEDIA TV bila kuwa na leseni ya mamlaka husika, kati ya Oktoba 14, 2017 na Septemba mosi, 2020 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Aidha, mshitakiwa amekana kutenda kosa hilo na amefanikiwa kutimiza masharti ya dhamana kama ilivyoamriwa na Mahakama.
Hata hivyo upande wa mashitaka umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo kuiomba Mahakama kupanga tarehe nyingine.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 20, 2020 itakapotajwa.