Waziri wa Ulinzi wa Marekani Mark Esper amekanusha kwamba Ikulu ya nchi hiyo ilikuwa inajiandaa kuyaondoa majeshi yake Iraq.
Tangazo hilo limetolewa baada ya Jenerali mwandamizi wa Marekani kumpa barua Jenerali mwenzake wa Iraq inayosema kuwa vikosi vya Marekani vitaondoka Iraq katika siku na wiki zijazo.
Mkuu wa kikosi cha Marekani nchini Iraq, Brigedia Jenerali William Seely alituma barua kwa kamandi ya operesheni ya pamoja nchini Iraq, nakala ambayo ilionekana na vyombo vya habari.
Barua hiyo imesema kuwa vikosi vya muungano vinavyoongozwa na Marekani kupambana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS vitachukua hatua kuhakikisha harakati za kuondoka Iraq zinafanyika mara moja na salama .