Mahakama yabariki ushindi wa Ruto

0
211

Mahakama ya Juu ya Milimani ya Kenya imesema hakuna ushahidi wa kutosha unaoweza kubatilisha matokeo ya Urais yaliyompa ushindi William Ruto kutoka muungano wa Kenya Kwanza.

Kufuatia hali hiyo, Mahakama hiyo imesema Ruto ni Rais Mteule halali wa Taifa hilo, hivyo taratibu nyingine zinaweza kuendelea.

Akisoma hukumu hiyo Jaji Mkuu wa Kenya, Martha Koome amesema uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Kenya Agosti 9 mwaka huu ulikua huru na haki.

Akisoma hukumu ya kesi hiyo iliyosikilizwa na majaii saba, Jaji Mkuu Koome amesema tuhuma kuhusu taarifa za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) zilidukuliwa hazina uthibitisho wowote.

Kesi hiyo ya kupinga matokeo ya Urais nchini Kenya ilifunguliwa na Raila Odinga aliyekuwa mgombea urais kupitia muungano wa Azimio la Umoja na mgombea mwenza wake Martha Karua.

Wawili hao walifungua kesi hiyo ya kupinga matokeo ya urais yaliyotangazwa Agosti 15 mwaka huu na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) Wafula Chebukati, huku wakidai kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu katika mchakato wa uchaguzi huo, hivyo matokeo hayo ya Urais ni batili.