Baadhi ya wakazi wa jimbo la Ituri katika jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wameripotiwa kukimbilia nchini Uganda kuepuka mapigano ya kikabila yanayoendelea katika jimbo hilo.
Taarifa kutoka nchini humo zinaarifu kuwa maelfu ya wakazi hao wameingia nchini Uganda kwa kuvuka ziwa Albert na kufika salama katika kambi ya muda ya wakimbizi iliyopo mpakani mwa DRC na Uganda, ambapo wamesema hawataondoka katika eneo hilo hadi hapo machafuko yatakapokomeshwa katika jimbo hilo la Ituri.
Hata hivyo jeshi la DRC pamoja na vikosi vya ulinzi vya umoja wa mataifa vimefika katika vijiji kadhaa vya jimbo hilo ili kuimarisha ulinzi katika maeneo hayo ambapo baadhi ya mashamba na nyumba kadhaa zimeteketezwa kwa kuchomwa moto katika mapigano hayo ya kikabila.