Wafanyakazi wa Idara ya Afya katika mji wa Beira nchini Msumbiji, moja kati ya miji iliyoathiriwa zaidi na kimbunga Idai, wanaendelea kuwatibu maelfu ya watu wanaogua ugonjwa wa kuhara, ugonjwa unaoelezwa kuwa ni dalili ya awali ya Kipindupindu.
Hadi sasa watu watano wamethibitika kuugua kipindupindu, lakini wafanyakazi wa afya wameelezea wasiwasi wao kuwa idadi hiyo inaweza kuongezeka.
Kwa mujibu wa takwimu za sasa za Idara ya Afya katika mji huo wa Beira, idadi ya watu wanaougua ugonjwa wa kuhara imefikia Elfu Tatu.
Mbali na kuwepo kwa ugonjwa huo wa kuhara katika mji wa Beira, Maafisa wa afya pia wamejiweka katika hali ya tahadhari kufuatia wasiwasi wa kuwepo kwa magonjwa ya malaria, homa ya matumbo na Kipindupindu.
Maelfu ya watu nchini Msumbiji wameachwa bila ya makazi na hawana huduma ya maji safi, kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na kimbunga Idai takribani wiki mbili zilizopita.