Maelfu ya watu katika miji ya London (Uingereza), Madrid (Hispania) na Istanbul (Uturuki) wamejitokeza mitaani kuandamana kupinga vita vya Gaza huku Israel ikiahidi kuendelea na mashambulizi yake huko Rafah, kusini mwa Gaza.
Wakipeperusha bendera ya Palestina na mabango, maelfu wameandamana katika mitaa ya Madrid, nchini Hispania wakitaka kusitishwa mara moja kwa mapigano katika Ukanda wa Gaza wakisema wanaoumia si askari bali raia.
Umati wa watu ulipenya katika mitaa iliyofungwa katika mji mkuu huo wa Hispania kutoka kituo cha treni cha Atocha hadi eneo la kati la Plaza del Sol, nyuma ya bendera kubwa iliyosomeka: Uhuru kwa Palestina.
Wengi wamebeba mabango yaliyosomeka “Amani kwa Palestina” na “Usipuuze mateso ya Wapalestina”.
Takriban mawaziri sita kutoka baraza la mawaziri la Waziri Mkuu, Pedro Sanchez pia wameshiriki katika maandamano hayo, watano kutoka chama cha mrengo wa kushoto cha Sumar, pamoja na Waziri wa Uchukuzi, Oscar Puente wa chama cha Waziri Mkuu cha Socialist Party.
“Tunahitaji kusitishwa kwa mapigano mara moja, kukomesha mauaji na mashambulizi dhidi ya raia wasio na hatia, lazima tufanikishe kuachiliwa huru kwa mateka wote,” Puente amewaambia waandishi wa habari mwanzoni mwa maandamano hayo.
Katika mji mkuu wa Uingereza, London, takriban watu 250,000 wameshiriki katika maandamano ya kutaka kusitishwa kwa mapigano huko Gaza, kulingana na Kampeni ya Mshikamano wa Palestina (PSC).
Akiripoti kutoka London, mwandishi Harry Fawcett wa Al Jazeera amesema maandamano yanayofanyika London ni kati ya matatu kwa ukubwa tangu kuanza kwa vita huko Gaza mnamo Oktoba.
Maandamano pia yamefanyika katika mji mkuu wa Israel, Tel Aviv na nje ya makazi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu huko Jerusalem Magharibi huku waandamanaji wakitaka kufikiwa kwa makubaliano ya kubadilishana wafungwa na kufanyika uchaguzi wa haraka nchini humo.
Maandamano hayo yamefanyika kufuatia uamuzi wa Netanyahu wiki iliyopita kutotuma ujumbe wa Israel mjini Cairo kwa ajili ya mazungumzo zaidi kuhusu makubaliano ya kuwaachilia zaidi ya mateka 100 ambao bado wanashikiliwa huko Gaza.
Baraza la Mateka na Familia Zilizotoweka liliuita uamuzi huo “hukumu ya kifo” kwa wafungwa waliosalia.
Lakini katika mkutano na wanahabari jana, Netanyahu alitupilia mbali uwezekano wa kufanyika kwa uchaguzi nchini Israel hivi sasa.