Macron ampa uraia mhamiaji aliyemuokoa mtoto aliyekuwa akining’inia ghorofani

0
1437

Mtoto wa miaka minne akining’inia kutoka ghorofa ya nne kabla hajaokolewa na mhamiaji kutoka nchi ya Mali Mamoudou Gassama (22). Picha ya pili Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa akizungumza na Gassama leo Jumatatu Mei 28. .

Mhamiaji kutoka Mali aliyekuwa ‘akibangaiza’ maisha huko Ufaransa, Mamoudou Gassama ghafla amejikuta mambo yake yakinyooka, baada ya Rais Emmanuel Macron kuagiza apewe uraia wa Ufaransa kwa kitendo cha kishujaa alichofanya mwishoni mwa wiki iliyopita, cha kukwea ghorofa kutokea nje hadi kufanikiwa kumuokoa mtoto aliyekuwa akininginia nusura aanguke, kutoka ghorofa ya nne.

Gassama amepata umaarufu mkubwa katika vyombo vya habari vya Ufaransa na duniani kuanzia Jumamosi iliyopita siku ambayo tukio hilo limetokea, kiasi kwamba Rais Macron amemuita Ikulu leo Jumatatu ambapo baada ya kuzungumza naye, Rais huyo akatangaza kuwa atapatiwa uraia wa Ufaransa.

Picha za video zilizochukuliwa na baadhi ya mashuhuda zimeonyesha jinsi Gassama ambaye alikuwa ni mpita njia, alivyopanda kwa kasi ghorofa hadi ghorofa kutokea nje ya jengo hilo huku akishangiliwa na mashuhuda wengine, hadi kumfikia mtoto huyo mwenye umri wa miaka minne na kufanikiwa kumweka mikononi mwake akiwa salama.

Gassama amesema wakati akipita njia katika eneo hilo kaskazini mwa jiji la Paris, aliona umati wa watu waliokusanyika mbele ya jengo hilo na kuongeza kuwa alihisi maumivu makali kumuona mtoto yule katika hali ile ndipo akachukua ujasiri wa kwenda kumuokoa.

“NIlipofanikiwa kumuweka kwenye mikono yangu nilizungumza naye na kumuuliza kwa nini umefanya hivi lakini hakunijibu” amesema Gassama.

Maofisa wa kikosi cha zimamoto cha Paris wamesema askari wao walipofika katika jengo hilo walikuta mtoto huyo alishaokolewa.

“Kwa bahati palikuwa na mtu ambaye ni mkakamavu kimaumbile na aliyekuwa na ujasiri wa kwenda kumuokoa mtoto huyo” msemaji wa zimamoto aliwaambia waandishi wa shirika la habari la AFP.

Viongozi wa mtaa tukio hilo lilipotokea wamenukuliwa wakisema kuwa wakati tukio hilo linatokea wazazi wa mtoto huyo hawakuwepo nyumbani.

Polisi wanamshikilia baba wa mtoto huyo kwa tuhuma za kumuacha mtoto bila uangalizi, ambapo inasemekana kuwa mama wa mtoto huyo alikuwa nje ya jiji la Paris wakati tukio linatokea.

Meya wa jiji la Paris Anne Hidalgo alikuwa ni mmoja wa watu waliompongeza Gassama(22) kwa kumpigia simu yeye binafsi na baadae kuongea na waandishi wa habari huku akimpachika jina la ‘spiderman’ akimaanisha mtu mwenye uwezo mkubwa wa kukwea majengo marefu.

Rais Macron amemshukuru Gassama na kumpa medali kwa ujasiri, lakini pia amesema Ufaransa itampa ajira ya uaskari shujaa huyo, katika kikosi cha zimamoto.