Kitambi dili

0
277

Katika kabila la Bodi nchini Ethiopia, wanaume hujiandaa kwa miezi sita kushiriki shindano la urembo.

Ndani ya miezi hiyo sita mwanaume hukaa ndani na kula vyakula maalum na kufuata ratiba maalum kama vile kunywa damu ya ng’ombe mapema jua linapochomoza, zoezi linaloonekana kuwa ni gumu lakini muhimu kwa wanaume hao.

Vilevile hunywa maziwa na pia hupaswa kuacha kabisa tendo la ndoa kwa wakati huo.

Yote hayo ni ili kukuza vitambi ambapo siku ya shindano washindani hupakaza udongo na majivu kwenye matumbo yao.

Wanaume wengine wanaripotiwa kuwa wanene sana hivi kwamba hawawezi kutembea vizuri, unene watakaohangaika kuupunguza baada ya shindano.

Wakati wa sherehe hiyo, ng’ombe huchinjwa, wanaume hutembea kwenye miduara kuzunguka mti mtakatifu, na wanawake huwapa pombe ili kuwachangamsha huku wakiwafuta jasho.

Washindani hupimwa matumbo yao na aliyenona zaidi na mwenye kitambi kikubwa zaidi huibuka mshindi na kuitwa mwanaume mzuri zaidi ‘handsome’ na shujaa wa maisha.

Cha kustaajabu ni kwamba kila kijana ana ndoto ya kuvikwa taji la mtu mnene zaidi.