Kipindupindu chaua 700 Zambia

0
207

Idadi ya vifo kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini Zambia imeongezeka hadi kufikia 700, linasema shirika la huduma za matibabu la Médecins Sans Frontières (MSF).

Idadi hiyo imeelezwa kuwa ni kubwa zaidi kuwahi kutokea nchini humo. Mlipuko wa ugonjwa huo ulianzia katika Jiji la Lusaka, mwezi Oktoba mwaka jana na tangu wakati huo kipindupindu kimeenea katika majimbo yote ya Zambia ambapo zaidi ya watu 19,000 wameugua ugonjwa huo.

MSF inasema kipindupindu kinatibika kwa urahisi endapo mgonjwa ataongezewa maji mwilini huku akipata dawa sahihi lakini kama hakuna uangalizi mzuri mtu anaweza kufa ndani ya saa chache.

Ugonjwa wa kipindupindu kwa sehemu kubwa husababishwa na kunywa maji yaliyochafuliwa na vijidudu vya ugonjwa huo na hivyo upatikanaji wa maji safi ya kunywa ni muhimu ili kuuzuia kuenea zaidi kwa kipindupindu.