Kiongozi wa wagner afariki dunia

0
545

Watu kumi wanaaminika kuwa wamefariki kwenye ajali ya ndege Kaskazini mwa Mji Mkuu wa Urusi, Moscow ambapo Mamlaka ya Anga ya Urusi imesema Kiongozi Mkuu wa Kundi la Wagner Yevgeny Prigozhin ni miongoni mwa abiria waliokuwemo kwenye ndege hiyo.

Itakumbukwa June 24,2023 Prigozhin, Mmiliki na Mwanzilishi wa Wagner alitoa wito wa uasi wa kutumia silaha na kutishia kufanya vurugu Jijini Moscow ili kumtimua Waziri ambaye alimtuhumu kwa kuamuru kulipuliwa kwa kambi za vita za wagner group nchini Ukraine na baadaye Ikulu ya Urusi (Kremlin) ikasema Prigozhin alikubali kwenda uhamishoni nchini Belarus hii ni baada ya Rais wa Urusi, Vladimir Putin kuafikiana na makubaliano ya msamaha kwa Kiongozi huyo ili kusitisha uasi.

Mzozo wa muda mrefu kati ya Prighozin na Viongozi wa kijeshi juu ya uendeshaji wa operesheni ya Urusi huko Ukraine ulishika kasi June mwaka huu, vikosi vya Wagner vilipochukua udhibiti wa kambi muhimu ya Jeshi la Urusi katika mji wa Rostov-on-Don.

Putin alishutumu hatua hiyo kama uhaini na kuapa kuwaadhibu Wahalifu, akiwatuhumu kwa kuisukuma Urusi kwenye ukingo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.