Kesi ya rushwa ya Zuma yaendelea kuunguruma

0
247

Kesi ya rushwa inayomkabili Rais wa zamani wa Afrika Kusini aliyepo gerezani Jacob Zuma, inaendelea leo kwa njia ya video.

Kesi hiyo inaendelea licha ya kuwepo kwa vurugu na maandamano katika maeneo mbalimbali nchini Afrika Kusini, ambapo Waandamaji hao wanapinga Zuma kufungwa jela miezi 15 katika kesi nyingine ya kudharau mahakama.

Zuma anakabiliwa na mashtaka 16 ya rushwa kuhusu ununuzi uliofanyika mwaka 1999 wa ndege za kivita, boti za doria na vifaa vya jeshi kutoka kwa kampuni tano za kijeshi barani Ulaya wakati akiwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo.

Anatuhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa moja ya kampuni hizo ambayo ni Thales ya nchini Ufaransa, ambayo ilishtakiwa kwa rushwa na utakatishaji fedha.

Kesi hiyo ilianza mwezi Mei mwaka huu baada ya kuahirishwa na kucheleweshwa mara kadhaa, wakati timu ya upelelezi ya Zuma ikipambana kutaka mashtaka hayo yafutwe.

Zuma mwenye umri wa miaka 79 amesisitiza hana hatia, huku kampuni ya Thales nayo pia ikikana mashtaka hayo.