Kauli ya Mwalimu Tabichi baada ya kupata Tuzo

0
326

Mwalimu wa Sayansi kutoka nchini Kenya, –  Peter Tabichi aliyeshinda tuzo ya kuwa Mwalimu bora Duniani na kupatiwa zawadi ya Dola Milioni Moja za Kimarekani, amewataka walimu duniani kote kujitolea, kufundisha kwa moyo na kutotanguliza mbele maslahi yao.

Katika mahojiano yake na Shirika la Utangazaji la BBC, Mwalimu Tabichi aliyeshinda tuzo hiyo ya Dunia ya mwaka 2019 ya Mwalimu Bora amesisitiza kuwa kazi ya Ualimu ni wito na kila mtu aliyejitoa kufanya kazi hiyo ni lazima aonyeshe mapenzi makubwa kwa anaowafundisha.

Mwalimu Tabichi anayetoka kwenye  Shirika la Kidini la Francisco na kufundisha  katika shule ya sekondari ya Kericho huko Nakuru amesema kuwa,  bila ya wito huwezi kufanya kazi ya Ualimu kwa kuwa mwalimu anakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya  umaskini.

Tabichi amekua akitumia asilimia 80 ya mshahara wake kila mwezi kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi maskini zaidi  katika shule hiyo ya  sekondari ya Keriko.

Tuzo hiyo ya Dunia ya mwaka 2019 ya Mwalimu imetolewa katika sherehe zilizofanyika mjini Dubai, ambapo Mwalimu Tabichi ametambuliwa kama mtu aliyejitolea kufanya kazi zisizo za kawaida kwa wanafunzi katika eneo lisiloweza kufikiwa kwa urahisi la bonde la Ufa nchini Kenya.