Kahawa za mamilioni zilizoibwa Tanzania zakamatwa Kenya

0
341

Jeshi la polisi katika Kaunti ya Kajiado nchini Kenya limekamata magunia 270 ya kahawa zenye thamani ya Tsh 34 milioni ambazo zinadaiwa kuibwa nchini Tanzania.

Kamanda wa polisi katika kaunti hiyo, Daudi Lonyorokwe amesema inaaminika kuwa kahawa hizo ziliingizwa kinyemela nchini kupitia mpaka wa Namanga.

Mzigo huo ulikamatwa ukisafirishwa kwenye lori lenye namba za usajili KCA 206D likielekea jijini Nairobi.

Dereva wa lori hilo Stephen Njuguna anashikiliwa na amepelekwa katika Kituo cha Polisi cha Kajiando huku uchunguzi wa sakata hilo ukiendelea.

Kwa mujibu wa jeshi la polisi dereva huyo hakuweza kuonesha nyaraka za msingi za mzigo huo pindi alipokamatwa.