Mwanamuziki raia wa Canada, Justin Bieber (28) amefichua kuwa anaugua ugonjwa wa kupooza usoni baada ya matamasha yake kuahirishwa wiki hii.
Justin amethibitisha hayo kwenye video fupi katika ukurasa wake wa Instagram ambao una wafuasi milioni 240, kwamba hali hiyo ni kutokana na kugunduliwa kuwa ana ugonjwa unaoitwa Ramsay Hunt.
“Kama unavyoona jicho langu halikonyezi, siwezi kutabasamu upande huu wa uso wangu… Kwa hiyo kuna kupooza kabisa upande huu wa uso wangu,” amesema.
Mapema wiki hii, Bieber’s Justice World Tour – iliyoanza Februari – ilitangaza matamasha matatu ambayo yameahirishwa.
“Ni kutokana na virusi hivi vinavyoshambulia mishipa ya fahamu katika sikio langu na mishipa ya usoni na kusababisha uso wangu kupooza,” mwimbaji huyo alielezea kwenye video hiyo ya dakika tatu, akionesha upande wa kulia wa uso wake.
Pia Justin ameomba mashabiki wake wawe na subira, na akasema kuhusu maonyesho yake yajayo kwamba “kimwili, ni wazi, sina uwezo wa kuyafanya tamasha”. Alithibitisha kwa kujaribu kutabasamu na kupepesa macho, akiwaonyesha jinsi upande wa kulia wa uso wake haukusogea.
https://www.instagram.com/tv/CeorE9OjqX9/?utm_source=ig_web_copy_link
“Hii ni mbaya sana, kama unavyoona. Natamani isingekuwa hivyo, lakini, ni wazi, mwili wangu unaniambia lazima nipunguze,” alisema. “Natumai mmeelewa. nitatumia muda huu kupumzika ili kurejea kwa asilimia mia moja ili nifanye kile nilichozaliwa.”
Bieber aliongeza kuwa amekuwa akifanya mazoezi ya uso ili “kurejea katika hali yake ya kawaida”, lakini hajui itachukua muda gani kupona.
Kulingana na Kliniki ya Mayo nchini Marekani: “Mbali na upele ugonjwa wa Ramsay Hunt unaweza kusababisha kupooza kwa uso na kupoteza kusikia katika sikio lililoathirika.” kwa watu wengi, dalili za ugonjwa wa Ramsay Hunt ni za muda mfupi, lakini zinaweza kudumu.
,kutoweza kwa wagonjwa kufunga kope moja kunaweza pia kusababisha maumivu ya macho na kutoona vizuri, shirika hilo linasema, na kuongeza kuwa ni kawaida kwa watu zaidi ya miaka 60.
Mwezi Machi, mke wa mwanamuziki huyo, Hailey Bieber, alilazwa hospitalini kutokana na kuganda kwa damu kwenye ubongo wake.
Baadaye alisema alipatwa na kiharusi na alifanyiwa upasuaji wa kuziba tundu kwenye moyo wake.