Jeshi lataka Bouteflika aondolewe madarakani

0
307

Mkuu wa Majeshi wa nchini Algeria
Luteni Jenerali Gaed Salah ametaka Rais wa nchi hiyo Abdelaziz Bouteflika kutangazwa kuwa hawezi kuongoza tena taifa hilo kutokana na sababu za kiafya.

Akilihutubia Taifa kupitia kituo cha Televisheni cha Serikali, Luteni Jenerali Salah amesema kuwa ni lazima lipatikane suluhisho la jambo hilo haraka iwezekanavyo ili kumaliza maandamano yenye lengo la kumtaka Bouteflika
aondoke madarakani.

Maandamano hayo yalianza mwezi mmoja uliopita, baada ya Bouteflika mwenye umri wa miaka 82 kutangaza mpango wake wa kuwania urais kwa muhula mwingine .

Hata hivyo, tayari Bouteflika ametangaza hatowania muhula wa Tano wa Urais katika uchaguzi mkuu ujao ambao umesogezwa mbele.

Mkuu huyo wa Majeshi wa Algeria ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo amesisitiza kuwa katiba kitu pekee kitakachoamua hatma ya uongozi wa nchi hiyo.

Luteni Jenarali Salah ametaka kutumika kwa kifungu cha 102 cha katiba ya Algeria, kifungu kinacholiruhusu Baraza la Kikatiba nchini humo kutangaza nafasi ya Urais iko wazi endapo kiongozi wake hawezi kuongoza.