Japan imeahidi kutoa dola bilioni 30 za kimarekani ili kuziwezesha nchi za Afrika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, na kuimarisha utunzaji wa mazingira.
Ahadi hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida wakati wa mkutano wa nane wa Kimataifa wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaohusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD 8) unaofanyika jijini Tunis, Tunisia.
Akizungumza kwa njia ya mtandao na viongozi hao Kishida amesema, fedha hizo zitatolewa kwa kipindi cha miaka mitatu, ili kuimarisha utunzaji wa mazingira, uwekezaji hasa kwa vijana, sekta za afya, viwanda na elimu.
“Ijapokuwa siko pamoja nanyi kwenye mkutano huo, bado dhamiri yangu ya kuendeleza bara la Afrika iko palepale, haijabadilika, kwa kuanzia, Japan itaanzisha Japan’s Green Growth Initiative with Africa ambapo itatoa dola za Marekani bilioni nne kwa taasisi za umma na za binafsi barani Afrika ili kuziwezesha kutekeleza mpango huo.” amesema Waziri Mkuu Kishida
Amesema Japan imelenga kukuza uwekezaji, ambapo safari hii wamelenga kuwainua vijana.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu huyo wa Japan, vijana watakaolengwa zaidi ni wale wanaoanzisha kampuni na kwamba hatua hiyo itawapa fursa vijana wa Afrika na wa Japan kufanya kazi kwa karibu.