Baada ya mchakato wa kumwondoa madarakani Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua jana usiku na kisha suala hilo kuandikwa rasmi kwenye gazeti la Serikali, Rais William Ruto anatazamiwa kuchagua mrithi wa Gachagua muda wowote kuanzia sasa.
Wakati kuna habari kwamba Bunge la Kitaifa la Kenya linajiandaa kukutana leo pengine kwa sababu ya kujadili na kupitisha jina litakalopendekezwa, kuna tishio pia la mawakili wa Gachagua kutinga mahakamani kupinga mchakato wa kupitisha na hatimaye kuapishwa kwa Naibu Rais mpya.
Hata hivyo, kuna majina kadhaa yanatajwa kwamba miongoni mwao ndimo anatazamiwa kutoka Naibu Rais mpya wa Kenya. Miongoni mwa majina hayo ni:
- Profesa Kithure Kindiki – Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa. Kindiki anatajwa sana kutokana na sifa zake za uongozi, na alionekana kuwa mshirika mkuu wa Ruto wakati wa kampeni za urais. Hata hivyo, Kindiki ana sifa nyingine ya kuwa Mkikuyu anayetokea katikati mwa Kenya (Mlima Kenya) ambako ndiko kuna wapiga kura wengi na watu wenye uchumi mkubwa nchini humo.
- Musalia Mudavadi – Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri. Mudavadi, mwenye uzoefu mkubwa serikalini, anaungwa mkono na baadhi ya wanasiasa wa Magharibi ya Kenya, wakimtaja kama mtu anayefaa zaidi kuchukua wadhifa huo kutokana na historia yake ya kushika nafasi kubwa kubwa serikalini.
- Anne Waiguru – Gavana wa Kirinyaga, anayekubalika na baadhi ya viongozi kutoka eneo la Mlima Kenya. Wengine wanatamani kuona mwanamke pia anashika wadhifa wa juu wa uongozi wa serikali ya Kenya.
- Ndindi Nyoro – Mbunge wa Kiharu, pia anatajwa kutokana na umaarufu wake ndani ya chama tawala.
Majina mengine yanayojadiliwa ni pamoja na Kimani Ichung’wa, Irungu Kang’ata, na Alice Wahome, wote wakiwa viongozi mashuhuri kutoka Mlima Kenya.