Hali ya kawaida yarejea Nairobi

0
979

Umoja wa Afrika -AU na Umoja wa Mataifa – UN wamelaani vikali shambulio la kigaidi lililotokea katika hoteli ya Dusit mjini Nairobi nchini Kenya, Jumanne Januari 15 na kutuma salamu za pole kwa waliofiwa na kuwatakia nafuu ya haraka waliojeruhiwa.

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat amesema shambulio hilo linakumbusha umuhimu wa kudhibiti ugaidi barani Afrika.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani hilo na kusema yuko pamoja na watu wa Kenya na serikali yao.

Katika hatua nyingine Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ametangaza kuwa watu wote waliohusika na shambulio la kigaidi katika hoteli ya Dusit mjini Nairobi na kuwashikilia watu kadhaa mateka kwa saa 20 wameuawa na hali ya utulivu imerejea nchini humo.

Kenyatta amelihutubia taifa hilo leo asubuhi na kutangaza kuwa watu kumi na wanne wamekufa, baada ya watu hao wenye silaha kushambulia hoteli hiyo na kuanza kufyatua risasi. Watu zaidi ya mia saba waliokuwa katika eneo hilo la hoteli wameokolewa.

Viongozi wa upinzani nchini Kenya wamewasifu maafisa usalama nchini humo waliofanya juhudi kuwadhibiti watu hao wenye silaha na kuweza kulidhibiti tukio hilo kwa haraka.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amesema washambuliaji hawakuangalia tabaka, bali shambulio lao lililenga kila mtu hivyo ni vema wananchi wa Kenya kuungana ili kupambana na vitendo vya ugaidi.