Mazishi ya raia wa Marekani mwenye asili ya Afrika George Floyd ambaye alifariki dunia akiwa mikononi mwa polisi, yanafanyika leo nyumbani kwao katika mji wa Houston uliopo kwenye jimbo la Texas nchini Marekani.
Kabla ya mazishi hayo, jeneza lililobeba mwili wa Floyd liliingizwa katika Kanisa la The Fountain of Praise huku maelfu ya waombolezaji wakiwa kwenye mstari kusubiri kutoa heshima zao za mwisho.
Baadhi ya watu waliofika kanisani hapo wamesikika wakisema wanataka mauaji ya watu weusi nchini Marekani yawe historia, huku wengine wakisifu umoja uliooneshwa na raia wa nchi hiyo kufuatia kifo cha Floyd.
Kaka wa George, – Philonise Floyd amesema familia haitachoka kutafuta haki kufuatia kifo cha mdogo wake.
Wakati mazishi ya Floyd yakifanyika, mtuhumiwa mkuu wa mauaji yake Derek Chauvin ambaye tayari amefunguliwa mashitaka ya mauaji, ameachiwa kwa dhamana ya dola milioni moja za Kimarekani.