FIFA yafafanua kuhusu dakika za nyongeza

0
183

Kumezuka maswali mengi kwa nini muda wa nyongeza baada ya dakika 90 kumalizika umekuwa mwingi katika michuano ya FIFA ya Kombe la Dunia inayoendelea hivi sasa kulinganisha na ilivyozoeleka katika michuano mingine ya soka ngazi ya klabu.

Kutokana na maswali hayo kamati ya mashindano ya Kombe la Dunia imeeleza kuwa hali hiyo inatokana na muda unaopotea wakati wa mchezo husika na hivyo kulazimika kufidiwa baada ya dakika 90 za kawaida.

Michezo minne iliyopigwa mpaka jana imeshuhudia muda mwingi ukiongezwa katika michezo yote huku mchezo baina ya England na Iran zikiongezwa dakika 17 na sekunde 16.

Kamati hiyo imesema, muda huo unatokana na kuumia na kutibiwa kwa wachezaji uwanjani, muda unaopotea wakati wa kuhakiki matukio kwenye VAR, muda wa mabadiliko ya wachezaji na muda unaopotezwa na wachezaji kwa hila wakati mchezo ukiendelea.

Mchezo wa ufunguzi kati ya wenyeji Qatar na Ecuardo ziliongezwa dakika 10 na sekunde 18, Senegal Vs Uholandi zimeongezwa dakika 12 na sekunde 49 na mchezo wa Marekani Vs Wales zimeongezwa dakika 14 na sekunde 34.

Wadau wengi wamehoji kuhusu muda huo wa nyongeza na baadhi hawakuwa na majibu kwanini dakika za nyongeza zimekuwa zaidi ya 10 tofauti na ilivyozoeleka katika michezo ya ngazi ya klabu na timu za Taifa .