Ethiopia na Somalia kuwakabili Al Shabaab

0
1162

Ethiopia  na Somalia  zimekubaliana kuunganisha nguvu ili kupambana na wanamgambo wa Al Shabaab wa nchini Somalia ambao wameendelea kuhatarisha usalama wa nchi hizo na nchi nyingine jirani.

Mataifa hayo yamefikia makubaliano hayo baada ya wanamgambo hao kufanya shambulio katika kambi moja ya kijeshi nchini Somalia na kusababisha vifo vya askari kadhaa, kabla ya kushambuliwa na vikosi vya Marekani.

Wanamgambo hao wa Al Shabaab,  wiki iliyopita walifanya mashambulio nchini Kenya na kusababisha vifo vya watu 21 na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Habari zaidi kutoka nchini Kenya zinasema kuwa watuhumiwa watano katika shambulio hilo ambalo ni la kigaidi  wamefikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka ya kuhusika na ugaidi.

Raia wa Kenya wameendelea kuwa na wasiwasi baada ya kubainika kuwa magaidi wanne kati ya watano waliohusika na shambulio hilo lililotokea mjini Nairobi ni raia wa nchi hiyo.