Dkt.Mpango Asisitiza Malezi kwa Watoto wa Afrika

0
701

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amewataka wazazi wote Afrika kujitahidi kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni pamoja na kuzungumza nao, ili kuweza kutatua changamoto wanazopitia na kuwasaidia kutumia maarifa, ujuzi na vipaji walivyonavyo.

Makamu wa Rais amesema hayo alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa mkutano wa 13 wa Kanda ya Afrika wa Jumuiya za Skauti wa Kike unaofanyika mkoani Dar es Salaam.

Pia amewasihi viongozi wa dini pamoja na wale wa kimila kushirikiana na serikali katika kulea watoto kimaadili, ili kuepusha vitendo viovu na visivyopendeza katika jamii.

Makamu wa Rais amesema Jumuiya za Skauti wa Kike katika mataifa ya Afrika zinapaswa kushirikiana na serikali zao pamoja na wazazi hasa wakati huu wa utandawazi, ili kuepusha vitendo vya mmomonyoko wa maadili.

Amezipongeza Jumuiya za “Girl Guides” barani Afrika kwa kuendelea kutetea haki za watoto wa kike na wanawake kwa ujumla, kuwajengea uwezo wa kujiamini pamoja na kutengeza viongozi wenye maadili mema waliochangia kuleta maendeleo barani Afrika.

Mkutano huo wa siku tano wa Jumuiya za Skauti wa Kike kanda ya Afrika ni mkutano wa kikatiba ambao hufanyika kila baada ya miaka mitatu.

Mkutano huo unawakutanisha wajumbe wa taasisi za guiding kutoka nchi 33 za Bara la Afrika ukiwa na kauli mbiu isemayo Tustawi Pamoja.