Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, leo Novemba 16,2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa Singapore Heng Swee Keat, mazungumzo yaliyofayika katika ukumbi wa Treasury 100 eneo la Shenton way Nchini Singapore.
Katika Mazungumzo hayo Makamu wa Rais amemkaribisha Naibu Waziri Mkuu huyo Tanzania na kumueleza kwamba Tanzania imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji pamoja na ufanyaji biashara. Makamu wa Rais amemueleza Naibu Waziri Mkuu kwamba Tanzania imejaaliwa rasilimali nyingi na za kipekee na hivyo kuwa na fursa kubwa ya kuwekeza katika sekta mbalimbali kama vile Nishati, Viwanda, Madini, Utalii pamoja na Mifugo.
Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu wa Singapore Heng Swee Keat amesema nchi ya Singapore ilichukua hatua mbalimbali ili kufikia maendeleo ya haraka ikiwemo kuvutia wawekezaji kutoka nje ya nchi pamoja na kujenga mahusiano na ushirikiano na nchi zilizoendelea.
Amesema nchi ya Singapore iliweka mkazo katika kutunga sera imara zisizobadilika mara kwa mara pamoja na kuweka sheria zinazolinda biashara pamoja na uwekezaji. Aidha ameongeza kwamba Nchi ya Singapore iliwekeza zaidi katika elimu hasa katika kupata walimu bora na kuweka mkazo katika elimu ya ufundi.
Aidha Naibu Waziri Mkuu wa Singapore ametaja Sekta ya Bandari kama sekta muhimu ilioharakisha zaidi maendeleo ya nchi hiyo na kuongeza kwamba tayari maboresho katika bandari hiyo yamewezesha shughuli zote za bandari kufanyika kwa kutumia mitambo maalum kuliko watu pamoja na kuwa na mtandao na bandari zingine duniani na masoko makubwa.