Dhoruba zatishia maisha Ufilipino, Marekani

0
2456

Serikali ya Ufilipino imeanza kuhamisha maelfu ya watu, kusambaza idadi kubwa ya wanajeshi na kuweka vituo vya huduma za dharura, ili kukabiliana na kimbunga cha ‘Mangkhut’, kinachotishia maisha ya watu takribani milioni 4, Kaskazini mwa nchi hiyo.

Kimbunga cha Mangkhut, ambacho ni kikubwa kuliko ‘Florence’ kinachoishambulia pwani ya Mashariki ya Marekani kwa sasa hivi, kinatarajiwa kutua katika kisiwa cha Luzon mapema kesho Jumamosi, ambapo kwa sasa kasi ya upepo ni kilomita 285 kwa saa.

Kimbunga hicho kilichotokana na dhoruba kali baharini, kimesababisha tahadhari kutolewa katika nchi zilizoko kwenye eneo lote la Mashariki na Kusini Mashariki mwa bara la Asia. Imeelezwa kuwa dhoruba ya pili iliyopewa jina la ‘Barijat’, pia imeshambulia eneo hilo.

Tayari Mangkhut imeharibu miundombinu huko Guam na visiwa vya Marshall vilivyoko katika bahari ya Pacific, na kusababisha mafuriko makubwa.

Hadi leo Ijumaa sehemu kadhaa za Guam zilikuwa bado hazina umeme.

Huko Marekani zaidi ya watu 100 wameokolewa kufuatia mafuriko yaliyotokana na kimbunga Florence katika mji wa New Bern, jimbo la North Carolina.

Taarifa zimesema kuna watu wengine wasiopungua 150 ambao bado wanasubiri kuokolewa kutoka kwenye maji.

Mji wa New Bern umefunikwa na maji kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha.

Mamlaka ya Hali ya hewa nchini Marekani imesema kuwa kimbunga hicho kitaleta mvua kubwa zaidi ya kuhatarisha maisha ya watu.