Daktari matatani kwa kuweka sumu kwenye dripu

0
692

Daktari mmoja huko Texas nchini Marekani anadaiwa kuingiza sumu kwenye mifuko ya dawa ‘dripu’ na kusababisha kifo cha daktari mwenzake na matatizo ya moyo kwa wagonjwa 11.

Daktari huyo Raynaldo Rivera Ortiz Jr (59) aliyebobea kwenye eneo la ganzi na usingizi amefanya tukio hilo ikiwa ni
hatua ya kulipiza kisasi kutokana na uchunguzi uliofanywa dhidi yake kuhusu utovu wa nidhamu.

Raynaldo alikamatwa Septemba 15 mwaka huu, wiki moja tangu bodi ya Matibabu ya Texas kumnyang’anya leseni baada ya wagonjwa waliokuwa na maendeleo mazuri hali zao kubadilika ghafla.

Inadaiwa kuwa mara baada ya daktari huyo kuchanganya sumu na dawa za wagonjwa, alikwenda kuzihifadhi katika jokofu ambapo wauguzi walizichukua na kuzitumia pasipo kujua kuwa zimewekwa sumu.

Picha mbalimbali za video ambazo zinamuonesha daktari huyo akiwa katika matukio ya kuchanganya dawa pamoja na sumu zimechezwa katika kikao cha mahakama mjini Texas, ambapo waendesha mashtaka mahakamani hapo wamemtaja Raynaldo kama ‘gaidi wa matibabu.’

Mahakama imetamka kuwa endapo Raynaldo ataachiwa kwa dhamana, anaweza kujihusisha na tabia ya ukatili ya kulipiza kisasi dhidi ya wale wanaohusika katika uchunguzi wa makosa yanayomkabili hivi sasa.