Rais Samia Suluhu Hassan ambaye leo anahitimisha ziara yake ya kiserikali nchini China, jana ameshuhudia utiaji saini wa mikataba na hati za makubaliano ya kimkakati 15 akiwa na mwenyeii wake Rais Xi Jinping.
Miongoni mwa mikataba hiyo ni ile inayolenga kuimarisha ushirikiano, biashara na uwekezaji baina ya mataifa hayo mawili.
Mikataba na makubaliano yaliyotiwa saini kati ya Tanzania na China ni kuhusu mahitaji ya kuwepo na soko kubwa la usafirishaji wa parachichi kutoka Tanzania kwenda China, mkataba unaohusu msaada wa RMB milioni 100 za ushirikiano wa kiuchumi na kitaalamu na mkataba kuhusu mahitaji ya kuwepo na soko kubwa la usafirishaji wa mabondo ya samaki pamoja na bidhaa nyingine za uvuvi kutoka Tanzania kwenda China.
Ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini pia imeshuhudia nchi hiyo ikiipunguzia Tanzania sehemu ya deni lake lenye thamani ya shilingi bilioni 31.4.
Aidha, China imetoa mkopo wenye masharti nafuu kwa Tanzania ambao thamani yake ni dola milioni 56.72 za kimarekani kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa uwanja wa ndege wa Zanzibar, Terminal II.
China ndio nchi inayoongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania ambapo hadi kufikia mwezi Oktoba mwaka huu ilikuwa na jumla ya miradi 1,098 yenye thamani ya dola bilioni 9.6 za kimarekani iliyosajiliwa katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Uwekezaji huo umefanyika katika sekta za viwanda, kilimo, mawasiliano, madini na uvuvi na kuzalisha ajira 131,718.