Wapiga kura nchini Botswana wameonekana kutokuwa upande wa chama tawala, hali ambayo inachukuliwa kama mtikisiko mkubwa wa kisiasa katika taifa hilo la Kusini mwa Afrika lenye utajiri mkubwa wa madini ya almasi.
Chama cha Botswana Democratic Party (BDP) – ambacho kimekuwa madarakani tangu uhuru mwaka 1966, kimeshinda kiti kimoja pekee cha bunge kufikia leo asubuhi. Hii inaonekana kwamba ushindi unakiendea chama cha upinzani cha Umbrella for Democratic Change (UDC).
Rais Mokgweetsi Masisi amekubali matokeo, akisema ni wazi kwamba chama chake kimepoteza “kwa kiwango kikubwa.” Licha ya kusimamia mabadiliko makubwa nchini Botswana, ukuaji wa kiuchumi usioridhisha na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira vinadaiwa kupunguza umaarufu wa BDP.
“Nitajiondoa kwa heshima na kushiriki katika mchakato wa mpito kabla ya kuapishwa kwa rais mpya,” Masisi amesema katika mkutano na waandishi wa habari leo Ijumaa. Amewataka wafuasi wa chama chake kubaki watulivu na kuunga mkono serikali mpya.
UDC inayoongozwa na wakili wa haki za binadamu, Duma Boko, imeshinda viti 25 mpaka asubihi hii kulingana na matokeo ya awali. Chama hicho kinatarajiwa kufikisha kiwango cha viti 31 kinachohitajika kwa ajili ya kupata wingi wa kura bungeni. Kimeahidi kupitisha mkakati mpya wa kiuchumi unaozalisha ajira zenye malipo mazuri na kugawa mali kwa njia inayowafaidi wananchi wote.
Kgoberego Nkawana, ambaye amechaguliwa kama Mbunge wa UDC, ameambia BBC kwamba vijana wengi nchini Botswana bado hawana ajira licha ya nchi hiyo kuongoza uzalishaji wa almasi duniani pamoja na sekta ya utalii inayokua kwa kasi. Chama hicho kimeahidi kutengeneza ajira 450,000 hadi 500,000 ndani ya miaka mitano.
Chama cha Botswana Patriotic Front (BPF), kinachoungwa mkono na Rais wa zamani wa nchi hiyo, Ian Khama ambaye alijitenga na BDP baada ya kutokea kutoelewana na Rais Masisi, kimepata viti vitano hadi sasa, wakati Chama cha Botswana Congress Party (BCP) kimepata viti saba. Kwa kuwa wabunge ndio wanaomchagua rais nchini Botswana, Boko yuko njiani kuwa mkuu mpya wa nchi mara tu Bunge litakapokutana kwa mara ya kwanza.
Wafuasi wa UDC wamekuwa wakisherehekea katika Mji Mkuu Gaborone na maeneo mengine ya nchi.