Chama cha Labour chapata ushindi mkubwa Uingereza

0
234

Sir Keir Starmer anatarajiwa kuchukua mikoba ya Rishi Sunak kama Waziri Mkuu mpya wa Uingereza baada ya chama chake cha Labour kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika jana.

Chama cha Labour kimepata viti 410 vya ubunge huku chama cha Conservative kikiambulia viti 131 tu kati ya viti 650, hatua inayokipa, chama hicho cha Labour uhalali wa kuunda Serikali.

Idadi hiyo ya viti vya ubunge kwa chama cha Conservative ambacho ni cha mrengo wa kulia inaelezwa kuwa ni ya chini zaidi kwa chama hicho kuwahi kupata kwa zaidi ya miaka 100.

Ushindi huo wa chama cha Labour, umemaliza takribani muongo mmoja na nusu wa utawala wa chama cha Conservative.

Huu ni uchaguzi wa kwanza wa kitaifa tangu Boris Johnson aliposhinda kwa kishindo kura ya mwaka 2019. Umefanyika baada ya Waziri Mkuu Rishi Sunak kuchukua hatua ya kushangaza ya kuitisha uchaguzi mkuu miezi sita mapema kuliko ilivyotakiwa.

Wakati wa kampeni Chama cha Sunak kilikuwa kikijitahidi kuwahakikishia wapiga kura kuhusu masuala kama vile kupanda kwa gharama ya maisha na malalamiko kuhusu huduma ya afya ya taifa.

Ushindi wa Labour maana yake ni kwamba Uingereza inarudi kwenye mrengo wa wastani wa kushoto baada ya karibu muongo mmoja na nusu wa serikali za mrengo wa kulia za chama cha Conservative.