CCM yamlilia mpigania uhuru Afrika Kusini

0
237

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Rais Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kwa Mwenyekiti wa chama cha African National Congress (ANC) cha nchini Afrika Kusini Gwede Mantashe na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, kufuatia kifo cha aliyekuwa Naibu katibu mkuu wa cha hicho Yasmin Jessie Duarte aliyefariki dunia tarehe 17 mwezi huu.

Katika salamu zake, Rais Samia amesema Jessie alikuwa mmoja wa viongozi imara wa ANC tangu enzi za mapambano ya kupinga ubaguzi wa rangi nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka imesema Rais amesema atamkumbuka kiongozi huyo kwa namna alivyokuwa anasimamia utu kwa ajili ya jamii yenye usawa bila kujali jinsia na rangi.

“Tuko pamoja na makomredi wote wa ANC, Afrika Kusini kwa ujumla, Afrika na kwingine kote duniani ambao mbali ya kuguswa na maisha ya kikazi ya Komredi Jessie, pia walishirikiana naye kwa namna moja au nyingine kutekeleza wajibu wa kizalendo, kupigania na kulinda uhuru wa Mwafrika na nchi za Afrika katika nyanja mbalimbali.”amesema Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa