Buyoya apinga waranti wa kukamatwa

0
1636

Rais wa zamani wa Burundi, -Pierre Buyoya amepinga waranti wa kukamatwa kwake uliotolewa na serikali ya nchi hiyo kwa madai ya kuhusika katika mauaji ya rais wa kwanza wa nchi hiyo aliyechaguliwa kidemokrasia, – Melchior Ndadaye na kusema kuwa hizo ni sababu za kisiasa.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Burundi ilitoa waranti wa kimataifa wa kukamatwa kwa Buyoya, maafisa wengine 11 wa zamani  wa nchi hiyo na raia  watano waliokuwa karibu naye kwa madai hayo ya kuhusika na  mauaji ya Ndadaye mwaka 1993.

Katika taarifa yake, Rais huyo wa zamani wa Burundi, – Pierre Buyoya  amesema kuwa ushahidi unaonyesha siasa ndizo zilizotumika katika kutoa waranti hiyo ili kuuficha mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini humo kwa sasa.

Kwa sasa Buyoya ni mwakilishi wa Umoja wa Afrika nchini Mali na ni mtu anayeheshimika sana Barani Afrika pamoja na nchi nyingine nje ya bara hilo.

Buyoya anayetokea kabila la Watutsi aliingia madarakani mwaka 1987 kwa kusaidiwa na jeshi la Burundi na aliachia wadhifa huo baada ya Ndadaye ambaye ni Mhutu kuchukua madaraka mwaka 1993.

Hata hivyo, Ndadaye aliuawa miezi minne baadae katika jaribio la mapinduzi lililofanywa na Wanajeshi wa Kitutsi wenye itikadi kali.