Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria amesema kuwa serikali yake itahakikisha uchaguzi mkuu unaofanyika hapo kesho unakua huru na wa haki.
Akilihutubia Taifa kupitia Televisheni ya nchi hiyo, Buhari amesema kuwa Nigeria ambalo ndilo Taifa imara zaidi kiuchumi Barani Afrika ni lazima lionyeshe mfano katika masuala ya kidemokrasi kwa kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika katika mazingira ya amani na utulivu.
Ametoa wito kwa Raia wote wa nchi hiyo na hasa vijana kutotumiwa na Wanasiasa kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani wakati wote wa upigaji kura na wakati wa kusubiri matokeo.
Katika uchaguzi huo, Rais Buhari anayewania muhula mwingine wa uongozi atapambana na kiongozi mkuu wa upinzani wa Nigeria, -Atiku Abubakar ambaye ni Mfanyabiashara tajiri na Makamu wa zamani wa Rais wa nchi hiyo.
Zaidi ya Raia Milioni 80 wa Nigeria wamejiandikisha kupiga kura katika uchaguzi huo Mkuu.