Sakata la kuanzishwa kwa ligi mpya ya soka Barani Ulaya itakayoitwa Ligi Kuu ya Ulaya (European Super League) limeendelea kuchukua sura mpya, baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza,- Boris Johnson kuungana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Ulaya (UEFA) na bodi ya Ligi Kuu ya Uingereza kupinga kuanzishwa kwa ligi hiyo.
UEFA imeonya kuwa wachezaji wanaohusika watapigwa marufuku kushiriki mashindano mengine yote katika ngazi ya nyumbani, Ulaya au ulimwengu na wanaweza kuzuiwa kuwakilisha timu zao za kitaifa.
Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limesema kuwa, halitatambua mashindano kama hayo na wachezaji wote wanaohusika katika mechi hizo wanaweza kunyimwa nafasi ya kucheza kwenye Kombe la FIFA la Dunia, huku likitoa wito kwa pande zote zinazohusika katika majadiliano kushiriki mazungumzo ya utulivu, yenye kujenga na yenye faida kwa mchezo wa soka.
Mashindano hayo yatakayokuwa yakifanyika katikati ya wiki, yameanzishwa na vilabu 12 vya mpira wa miguu vinavyoongoza katika ligi za Barani Ulaya.
Vilabu hivyo vilivyokubaliana ni Real Madrid, FC Barcelona, Atletico De Madrid, FC Internazionale Milano, AC Milan, Juventus, Arsenal, Chelsea, Liverpool, Manchester City, Manchester United, Tottenham Hotspur, huku vilabu vitatu vikitarajiwa kuongezeka.
Klabu za Bayern Munich, Borussia Dortmund na PSG zimekataa kujiunga na ligi hiyo.