Bobi Wine afutiwa mashitaka

0
2784

Serikali ya Uganda imemfutia mashitaka yaliyokua yakimkabili Mbunge wa jimbo la Kyadondo – Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.

Mbunge huyo ambaye aliwahi kuwa mwanamuziki nchini humo leo Agosti 23 alitarajiwa kurudishwa katika mahakama ya kijeshi iliyopo kwenye mji wa Gulu kaskazini mwa Uganda.

Kabla ya kuwepo kwa taarifa za kufutiwa mashitaka kwa Bobi Wine, mawakili wa Mbunge huyo walifahamishwa kuwa kesi yake itasikilizwa katika kambi ya kijeshi ya Makindye mahali anakozuiliwa mjini Kampala.

Vyombo vya dola nchini Uganda vimekua vikimshikilia Bobi Wine kwa madai ya kumiliki silaha kinyume na sheria, hatua iliyozusha maandamano katika maeneo mbalimbali nchini humo na kusababisha uharibifu wa mali huku wengi wa waandamaji hao wakisema kuwa tuhuma hizo zinahusiana na mambo ya kisiasa

Kumekuwa na shinikizo la kimataifa la kutaka kuachiliwa huru kwa Bobi Wine ambaye amekua akishikiliwa kwa takribani wiki moja, ikiwa ni pamoja na shinikizo kutoka kwa baadhi ya Wanamuziki maarufu duniani.