Ilikuwa ni kesi iliyovutia watu wengi Vietnam kutokana na kuhusisha moja ya utapeli mkubwa zaidi dhidi ya benki ambao pengine ni mkubwa kuwahi kutokea duniani.
Ndani ya ukumbi wa mahakama ya wazi iliyojengwa enzi ya ukoloni katika Jiji la Ho Chi Minh, mfanyabiashara mashuhuri mwenye umri wa miaka 67, leo Aprili 11, 2024 amehukumiwa kifo baada ya kupatikana na hatia ya kutumia ulaghai kuiibia benki kubwa zaidi nchini humo matrilioni ya pesa kwa kipindi cha miaka 11.
Anakuwa mmoja wa wanawake wachache sana nchini Vietnam kuhukumiwa kifo kwa uhalifu wa kutapeli taasisi za fedha.
Hukumu hiyo kali imetolewa kulingana kiwango cha utapeli kwa mujibu wa sheria za Vietnam. Truong My Lan amepatikana na hatia ya kutapeli Dola za Marekani bilioni 44 (zaidi ya shilingi trilioni 113) katika kipindi hicho kwa njia mikopo kutoka Benki ya Biashara ya Saigon.
Uamuzi huo unamtaka arejeshe Dola bilioni 27 ambazo waendesha mashitaka wamesema huenda zisipatikane tena. Wengine wanaamini kuwa hukumu ya kifo ni njia ya mahakama ya kujaribu kumfanya mwanamke huyo kurejesha baadhi ya matrilioni aliyokwapua kwa udanganyifu.
Katika kesi hiyo iliyotikisa nchi, takribani watu 2,700 waliitwa kutoa ushahidi, huku waendesha mashtaka 10 na mawakili wapatao 200 wakihusika.
Ushahidi ulikuwa katika masanduku 104 yenye uzito wa tani sita. Watu 85 walishtakiwa pamojavna Truong My Lan, ambao walikana mashtaka.
“Hakujawahi kuwa na kesi kama hii nadhani katika nchi hii ya kikokomunisti,” amesema David Brown, ofisa mstaafu katika serikali ya Marekani ambaye ana uzoefu wa muda mrefu nchini Vietnam.
Chanzo: BBC