Biden: Sijiengui na nitashinda

0
195

Biden: Sijiengui na nitashinda

Rais wa Marekani, Joe Biden amewatuliza Wanademokrati na timu yake ya kampeni akisema wasivunjike moyo kutokana na kutofanya vizuri kwenye mdahalo na mpinzani wake, Donald Trump wiki iliyopita na pia kuacha kuwasikiliza wanaomtaka ajiengue kwani anaamini atashinda uchaguzi wa Novemba.

Jana, Biden alikula chakula cha mchana na Makamu wa Rais, Kamala Harris katika Ikulu ya White House ambapo Biden aliweka wazi kuwa atasalia kwenye kinyang’anyiro hicho huku Harris akasisitiza kumuunga mkono.

“Mimi ndiye mteule wa Chama cha Demokrati. Hakuna mtu wa kuniondoa. Siondoki,” alisema Biden mbele ya timu yake ya kampeni.

Maneno hayo yalirudiwa katika barua pepe ya kuchangisha pesa iliyotumwa saa chache baadaye na wanakampeni wa Biden-Harris.

“Wacha niseme haya kwa uwazi na kwa urahisi niwezavyo: Ninagombea,” Biden alisema katika barua pepe hiyo, na kuongeza; “Nitakuwa kwenye kinyang’anyiro hiki hadi mwisho”.

Kutokana na baadhi ya wanachama wa Demokrati kuwa na wasiwasi hadi kumtaka ajiengue, kumekuwa na maswali iwapo mzee huyo mwenye umri wa miaka 81 ataendelea na kampeni au atajiondoa na kumpisha mtu mwingine kwani inawezekana lakini sasa ameweka wazi msimamo wake.

Katika mdahalo na mgombea wa chama cha Ripablikani, Trump, Rais Biden alionekana akibabaika mara kwa mara kujibu maswali na sauti yake ilikuwa dhaifu. Hilo lilizua wasiwasi katika chama chake kuhusu uwezo wake wa kushinda uchaguzi huo na hata kuendelea kuongoza taifa hilo kubwa.

Shinikizo la kumtaka Biden kujiuzulu pia limeongezeka kutokana na kura ya maoni ya New York Times iliyofanywa baada ya mjadala huo kuonesha kuwa Trump sasa anamzidi Biden kwa alama sita.

Lakini kura ya maoni tofauti iliyofanywa na CBS News ilionesha Trump akiwa na alama tatu tu mbele ya Biden katika majimbo muhimu.