Baba mzazi wa rapa Onika Tanya Maraj maarufu Nicki Minaj, Mzee Robert Maraj (64) amefariki dunia akiwa hospitalini alipokuwa akipatiwa matibabu kufuatia ajali ya gari huko jijini New York, Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi wa wa Kaunti ya Nassau, Robert Maraj alikuwa akitembea kati ya Barabara ya Roslyn na Raff Avenue Ijumaa jioni ndipo alipogongwa na gari lililokuwa likielekea ppande wa Kaskazini.
Polisi wanasema mara baada ya ajali hiyo kutokea, dereva alikimbia eneo hilo na bado anatafutwa. Baba wa Nicki Minaj alipelekwa katika hospitali akiwa katika hali mbaya na kupelekea kifo chake.
Hata hivyo, Nicki Minaj bado hajazungumza juu ya kifo cha baba yake haswa kwenye mitandao ya kijamii.
Mwanamuziki huyo na Baba yake hawakuwa na maelewano na haijulikani kama walipatana au la.
Mwaka 2010 Nicki Minaj aliweka wazi kuwa baba yake, alikuwa anakunywa sana pombe na alikuwa akitumia dawa za kulevya.