Aweso awajia juu walioshindwa kutatua changamoto ya maji

0
200

Waziri wa Maji Jumaa Aweso amewaondoa katika nyadhifa zao Watumishi waandamizi sita wa sekta ya maji mkoani Mtwara, kwa kile alichodai kuwa wameshindwa kutatua changamoto ya maji katika maeneo yao na kushindwa kufanya kazi kwa kushirikiana.

Watumishi hao walioondolewa katika nyadhifa zao ni Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Mtwara, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Mtwara (MTUWASA), Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Makonde, Meneja wa Ubora wa Maji mkoa wa Mtwara, Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Newala pamoja na Afisa manunuzi wa Mamlaka ya Maji Makonde.

Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara na wakazi wa mji wa Newala, Waziri Aweso ameeleza kusikitishwa na mwenendo usioridhisha wa Watumishi hao ambao wameshindwa kutatua changamoto ya maji kwa Wananchi na badala yake wamekuwa sehemu ya tatizo.

Ametumia mkutano huo wa hadhara kuwaomba radhi wakazi wa wilaya za Newala na Tandahimba mkoani Mtwara kwa adha ambayo wamekuwa wakiipata ya kukosa maji kutokana na Watumishi hao kuendeleza malumbano badala ya kufanya kazi waliyotumwa na Serikali ya kuwapatia maji safi na salama.